Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Asubuhi moja kila kitu kilionekana kuwa cha kawaida. Kulikuwa na chakula mezani kila siku na hakukuwa na sababu ya kufikiria jinsi kilivyofika hapo. Kazi ya kupika ilionekana kuwa jambo la kawaida sana lisilohitaji kujifunzwa kwa haraka.
Baada ya muda wa kucheza na kufanya shughuli mbalimbali njaa ilianza kugonga tumboni. Hatua za haraka zikaelekea jikoni kwa matumaini ya kukuta chakula tayari. Lakini safari hiyo iliishia kwenye mshangao mkubwa. Sufuria zilikuwa tupu na hapakuwa na mtu wa kuandaa chakula.
Macho yakatua kwenye mchele, unga na maharage yaliyokuwa jikoni. Wazo likazaliwa moyoni: “Kwa nini nisijaribu kupika mwenyewe?” Jiko likawashwa kwa tahadhari. Jaribio la kwanza halikufanikiwa sana. Chakula kilikaribia kuungua. Jaribio la pili lilikuwa bora kidogo. Kwa uvumilivu na umakini hatua kwa hatua chakula kikaanza kupikwa vizuri.
Muda si mrefu harufu nzuri ilijaza nyumba nzima. Kijiko cha kwanza nilipoonja chakula hicho tabasamu likachanua usoni. Furaha haikutokana na ladha pekee bali kutokana na ukweli kwamba chakula kile kilitokana na juhudi binafsi.
Tangu siku hiyo somo kubwa lilibaki akilini ujuzi ni rafiki wa maisha. Mtu anayejifunza kujitegemea huwa tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali. Na wakati mwingine mwalimu bora zaidi si kitabu wala darasa bali ni njaa yenyewe.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment