Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Migogoro ya wazazi ni hali ya kutokuelewana au mabishano
yanayotokea kati ya baba na mama katika familia. Migogoro hiyo inaweza kuwa ya
mara kwa mara au ya muda mfupi. Ingawa wazazi ndio wahusika wakuu wa migogoro
hiyo watoto nao huathirika kwa kiasi kikubwa. Hivyo migogoro ya wazazi ina
athari mbalimbali kwa watoto kiakili, kihisia na kijamii.
Migogoro ya wazazi husababisha watoto kuwa na msongo wa mawazo. Watoto wanapoona wazazi wao wakigombana mara kwa mara huishi kwa hofu na wasiwasi. Hali hii inaweza kuathiri afya yao ya akili na kuwafanya washindwe kuzingatia masomo au shughuli nyingine muhimu.
Pia migogoro ya wazazi huathiri maendeleo ya kielimu ya
watoto. Kutokana na mawazo mengi na mazingira yasiyo na utulivu nyumbani watoto
wanaweza kushindwa kufanya vizuri shuleni. Wengine hupoteza hamasa ya kusoma na
hata kushuka kitaaluma.
Aidha migogoro ya wazazi inaweza kusababisha watoto kuwa na
tabia zisizofaa. Baadhi yao huiga ugomvi wanaouona nyumbani na kutumia vurugu
au lugha mbaya wanaposhughulika na wenzao. Hali hii inaweza kuharibu mahusiano
yao na watu wengine katika jamii.
Vilevile migogoro mikubwa inaweza kusababisha kuvunjika kwa
familia kupitia talaka au kutengana kwa wazazi. Hali hii huweza kuwafanya
watoto kukosa malezi bora na upendo wa wazazi wote wawili jambo ambalo huathiri
ukuaji wao wa kimwili na kihisia.
Hata hivyo migogoro inaposhughulikiwa kwa hekima na
mazungumzo ya amani watoto wanaweza kujifunza namna ya kutatua tofauti kwa njia
nzuri. Hivyo wazazi wanapaswa kuwa makini katika kushughulikia migogoro yao ili
kulinda ustawi wa watoto.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872

Post a Comment