Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Amina alirudi nyumbani jioni ile akiwa na mwendo wa polepole tofauti na kawaida yake. Hakukuwa na haraka, hakuna kelele, hakuna tabasamu la kawaida alilozoeleka nalo.
Begani kulining’inia begi lake la shule lakini hata kuliondoa alichelewa. Alisimama kidogo mlangoni kabla ya kuingia ndani kana kwamba alikuwa akijipanga kukabiliana na kitu kisichoonekana.
Ndani ya nyumba kulikuwa na utulivu wa kawaida wa jioni. Sauti za mbali za majirani na harufu ya chakula kutoka jikoni.
Amina aliingia bila kusema neno. Alipita sebuleni akakaa kwenye kona kochi.
Hakuangalia simu, akuangalia TV na hakuangalia hata mlango.
Alikuwa tu pale kimya akiwa amejifunga ndani ya mawazo yake.
Mama yake alimuona muda mfupi baadaye. Hakusema chochote mara moja badala yake alitulia akimchunguza kwa mbali.
Kuna kitu kilikuwa tofauti. Sio uchovu wa kawaida wa shule ilikuwa ni mzigo usioonekana lakini mzito sana.
Amina aliinamisha kichwa kidogo mikono yake ikiwa imekunjwa juu ya mapaja. Macho yake yalionekana kama mtu ambaye amechoka kujaribu kueleza.
Sekunde zilipita bila maneno.
Ndani ya ukimya huo kulikuwa na historia nzima masomo ambayo hayakueleweka, shinikizo la kufuatilia wengine na hofu ya kuonekana hafai.
Alijaribu kuendelea kuwa “sawa” kwa muda mrefu. Lakini siku hiyo nguvu ya kujifanya ilifikia mwisho wake.
Alivuta pumzi ndefu polepole sana kana kwamba anajaribu kushusha mzigo alioubeba kwa muda mrefu bila msaada.
Hakukuwa na machozi mengi ala kelele. Ilikuwa uchovu wa ndani uliotulia juu ya uso wake.
Mama yake alisogea karibu na kukaa kimya pembeni yake bila kumlazimisha kusema chochote.
Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu Amina hakujisikia kama anapaswa kuficha kitu. Ukuta aliokuwa ameujenga ndani yake ulikuwa umeanza kupasuka taratibu.
Na katika ukimya huo wa chumba kulikuwa na mwanzo mdogo wa kuelewana sio kwa maneno bali kwa uwepo tu.Hakusema kitu lakina macho yake yalisema yote.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872




Post a Comment