SAUTI YA PEKEE ILIYOIBADILISHA MAISHA YA MTOTO MWENYE NDOTO KUBWA YA KUIMBA

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Sauti tamu ya mtoto mmoja ilisikika kila jioni katika mtaa wa Manzese jijini Dar es Salaam. Watu waliokuwa wakitoka kazini walisimama kwa muda kusikiliza uimbaji wake uliovutia masikio ya wengi. Mtoto huyo aliitwa Neema msichana mwenye umri wa miaka kumi na mbili aliyekuwa akisoma darasa la sita katika shule moja ya msingi jijini humo. Tangu akiwa mdogo Neema alipenda sana muziki na alitumia muda wake mwingi kuimba nyimbo mbalimbali kila alipopata nafasi.

Kila siku baada ya kurudi kutoka shuleni Neema alimaliza kazi zake za nyumbani kisha akaenda chumbani kwake kufanya mazoezi ya kuimba. Wazazi wake walifurahia kuona jinsi alivyokuwa akijituma kuendeleza kipaji chake. Mama yake alimtia moyo mara kwa mara na kumshauri asiogope kuonesha uwezo wake mbele ya watu. Ingawa baadhi ya marafiki zake walimcheka na kudhani alikuwa anapoteza muda Neema hakukata tamaa. Aliamini kuwa siku moja angeweza kufikia ndoto yake ya kuwa mwimbaji maarufu.

Siku moja uongozi wa shule yake ulitangaza mashindano ya vipaji kwa wanafunzi wote. Mashindano hayo yalilenga kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi katika maeneo mbalimbali kama vile uimbaji, uchoraji, ushairi na maigizo. Neema alifurahi sana kusikia tangazo hilo kwa sababu aliona kuwa ilikuwa nafasi nzuri ya kuonesha kipaji chake. Alianza kufanya mazoezi kwa bidii zaidi ili kujiandaa kwa siku ya mashindano.

Hatimaye siku ya mashindano ilifika. Wanafunzi wengi walijitokeza kuonesha vipaji vyao mbele ya walimu, wazazi na wanafunzi wenzao. Zamu ilipomfikia Neema alipanda jukwaani kwa ujasiri mkubwa. Alianza kuimba wimbo uliokuwa na ujumbe wa kuhimiza watoto kusoma kwa bidii. Sauti yake ilisikika kwa uwazi na uzuri mkubwa kiasi kwamba ukumbi mzima ulitulia huku watu wakimsikiliza kwa makini. Alipomaliza kuimba alipigiwa makofi mengi na hadhira yote.

Baada ya washiriki wote kumaliza maonesho yao majaji walitangaza matokeo. Neema alishinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha uimbaji. Ushindi huo ulimletea furaha kubwa yeye, familia yake na shule yake. Tangu siku hiyo alipewa nafasi ya kushiriki katika matamasha mbalimbali ya muziki na aliendelea kukuza kipaji chake.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments