Emakulata Msafiri
Mwanakwetu
Usiku ulikuwa kimya sana. Mwezi uliangaza dirishani mwa chumba kidogo cha mtoto mmoja aliyependa sana mdoli wake wa kitambaa. Kila siku alimshika karibu kana kwamba alikuwa rafiki wa kweli anayesikia na kuelewa kila jambo.
Siku hiyo kulikuwa na shamrashamra nyingi.Muziki ulisikika watoto walicheka na watu walijaa barabarani. Kwa furaha kubwa mtoto huyo alimchukua mdoli wake na kwenda kushuhudia sherehe.
Alikimbia huku na kule akicheza na watoto wengine mpaka jua lilipoanza kuzama. Ghafla mama yake alimwita warudi nyumbani. Kwa haraka aliondoka bila kujua kuwa kitu chake cha thamani zaidi kilikuwa kimebaki nyuma pembeni ya mti mkubwa.
Walipofika nyumbani ndipo moyo wake uliposhtuka.
Kitanda kilionekana tupu.Mikono yake ilitetemeka. Macho yakaanza kujaa machozi. Alitafuta kwenye kikapu, chini ya meza, nyuma ya mlangakini hakukuwa na mdoli.
Usiku huo hakulala mapema. Aliwaza mdoli wake akiwa peke yake gizani, akipigwa na upepo wa usiku. Alitamani angeweza kurudisha muda nyuma.
Asubuhi ilipofika aliamka mapema sana na kukimbia kuelekea kule kwenye sherehe ya jana. Kulikuwa kimya. Mabaki ya nyayo na karatasi zilizotapakaa ardhini pekee ndiyo yaliyoonekana.
Alianza kutafuta polepole huku moyo wake ukiwa mzito.
Mara akasikia sauti ndogo kutoka nyuma yake.
“Unamtafuta huyu?”Alipogeuka alimwona bibi mmoja akiwa ameshika mdoli wake. Kumbe aliukuta usiku ukiwa umeanguka karibu na mti akaamua kuuhifadhi ili mwenyewe aje kuuchukua.
Uso wake ulijaa furaha kuliko hata siku ya kupewa mdoli huo.
Aliukumbatia kwa nguvu kana kwamba alikuwa amempata rafiki aliyekuwa amepotea milele.
Tangu siku hiyo alijifunza kuwa vitu tunavyovipenda vinahitaji kutunzwa kwa makini kwa sababu wakati mwingine vinapopotea huacha pengo kubwa moyoni.
emakulatemsafiri@gmsil.com
0653903872



Post a Comment