MTOTO MWENYE UPENDO,ULINZI NA MALEZI BORA

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Mtoto ni zawadi muhimu katika familia na jamii. Ili mtoto aweze kukua vizuri anahitaji kupata upendo, ulinzi na malezi bora kutoka kwa wazazi, walezi pamoja na jamii inayomzunguka. Mtoto anayelelewa katika mazingira yenye amani na upendo huwa na furaha, afya nzuri na tabia njema.

Kwanza upendo ni msingi muhimu katika maisha ya mtoto. Mtoto anapopendwa hujisikia salama na kuthaminiwa. Wazazi wanapoongea vizuri na watoto wao kuwasaidia na kutumia muda pamoja nao watoto hupata furaha na kujiamini. Upendo huwasaidia watoto kukua wakiwa na moyo wa huruma na kuheshimu wengine.

Pia ulinzi wa mtoto ni jambo muhimu sana. Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili, mazingira hatarishi na tabia zinazoweza kuwaharibu. Familia na jamii zina wajibu wa kuhakikisha watoto wanaishi sehemu salama na wanapata mahitaji yao ya msingi kama chakula, mavazi, elimu na huduma za afya. Mtoto anayelindwa vizuri huwa na nafasi nzuri ya kufikia ndoto zake.

Aidha malezi bora humjenga mtoto kuwa raia mwema katika jamii. Wazazi na walezi wanapaswa kuwafundisha watoto maadili mema kama kusema ukweli, kuheshimu watu, kufanya kazi kwa bidii na kusaidia wengine. Malezi mazuri humsaidia mtoto kuwa na nidhamu na kuishi vizuri na watu wengine.

Hata hivyo baadhi ya watoto hukosa upendo na malezi bora kutokana na changamoto mbalimbali kama migogoro ya kifamilia, umaskini na ukosefu wa malezi sahihi. Hali hii inaweza kusababisha watoto kuwa na huzuni, kukosa mwelekeo mzuri wa maisha au kujiingiza katika tabia mbaya. Jamii inapaswa kushirikiana kuhakikisha kila mtoto anapata haki zake muhimu.

Kwa kumalizia mtoto mwenye upendo, ulinzi na malezi bora huwa na furaha na hukua vizuri katika jamii. Ni jukumu la wazazi, walezi na jamii nzima kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye upendo ili waweze kuwa viongozi bora wa kesho.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments