Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Musa alikuwa mvulana wa miaka kumi na miwili aliyeishi na bibi yake kijijini. Kila siku baada ya shule alimsaidia bibi kuchota maji, kufagia uwanja na kulisha kuku.
Siku moja mwalimu aliwaambia wanafunzi waandike barua kuhusu ndoto zao za baadaye. Wanafunzi wengi waliandika kwamba walitaka kuwa madaktari, marubani au walimu.
Musa aliandika "Nataka kuwa mhandisi ili nijenge daraja katika kijiji chetu. Wakati wa mvua watoto wengi hushindwa kwenda shule kwa sababu mto hujaa maji."
Wiki moja baadaye mwalimu alikusanya barua zote. Alivutiwa sana na mawazo ya Musa. Bila kumwambia alituma nakala ya barua hiyo kwenye mashindano ya uandishi ya wanafunzi yaliyofanyika wilayani.
Miezi miwili baadaye shule ilipokea taarifa kuwa Musa alikuwa mshindi wa pili. Alizawadiwa vitabu, daftari na ufadhili wa masomo kwa mwaka mmoja.
Musa alishangaa sana alipoitwa mbele ya wanafunzi wote kupokea zawadi yake. Alikumbuka siku aliyoandika barua ile akiwa ameketi kwenye dawati la mwisho darasani.
Alipofika nyumbani alimwonesha bibi yake vyeti na vitabu alivyopata. Bibi yake alifurahi sana hadi machozi yakamtoka.
"Musa alisema"usiogope kuota ndoto kubwa. Kila jambo kubwa huanza na wazo dogo."
Kuanzia siku hiyo Musa alijitahidi zaidi katika masomo yake. Hakujua kama angekuwa mhandisi lini lakini alijua kwamba alikuwa amepiga hatua moja kuelekea kwenye ndoto yake.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment