“HAKUTAFUTA UCHAWI LAKINI MUZIKI ULIMCHAGUA MWENYEWE”

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Usiku ulikuwa kimya sana kiasi kwamba hata sauti ya nyasi zikigusana ilisikika. Mwezi mkubwa ulitanda angani kama taa ya fedha huku watoto wengi wa kijijini wakiwa tayari wamelala.

Lakini kulikuwa na mtoto mmoja ambaye macho yake hayakupenda usingizi.

Kila usiku alikaa dirishani akiisikiliza dunia. Alisikia mbwa wakibweka kwa mbali kama ngoma nzito, bundi wakilia kama filimbi za porini na upepo ukipita kwenye miti kama wimbo wa siri.

Mtoto huyo alikuwa na tabia ya ajabu.

Badala ya kuchezea magari au mipira alikusanya vitu vilivyotupwa makopo ya zamani, vijiti vikavu, chupa tupu na waya zilizochakaa. Watu walidhani ni uchafu lakini mikononi mwake viligeuka vyombo vya muziki.

Siku moja akiwa kandokando ya mto alisikia sauti isiyo ya kawaida.

“Dum… dum… dum…”Haikuwa sauti ya mtu. Haikuwa radi. Ilikuwa kama moyo mkubwa wa dunia unapiga ndani ya ardhi.

Kwa hofu na hamu ya kujua akaifuata sauti hiyo mpaka akafika kwenye pango lililofunikwa na mizizi ya miti mikubwa. Ndani kulikuwa na giza lakini katikati ya pango palikuwa na ngoma kubwa ya ajabu iliyong’aa kwa mwanga wa buluu.

Alipoigusa tu sauti kubwa ilitokea na ghafla upepo mkali ukazunguka kijiji kizima. Miti ilianza kuyumba kama inacheza. Maji ya mto yakaruka juu kana kwamba yanaimba.

Kisha sauti nzito ikasikika kutoka gizani “Yule anayesikia muziki wa dunia ameiamsha ngoma ya kale…”

Mtoto yule alitetemeka.Hakuelewa kilichokuwa kinaendelea lakini tangu siku hiyo alianza kusikia midundo kila mahali kwenye mvua, kwenye hatua za watu hata kwenye mapigo ya moyo wake mwenyewe.Na kila alipopiga ngoma ile ya ajabu jambo fulani la kushangaza lilitokea.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments