Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Palikuwa na kijana mmoja mwenye bidii sana aliyekuwa akiishi maisha ya kujituma tangu utoto wake. Alipenda shule kuliko kitu chochote. Wakati watoto wengine wakicheza muda mwingi yeye alikesha akisoma chini ya taa ndogo ya mafuta huku akiamini kuwa elimu ndiyo ingembadilisha maisha yake na ya familia yake.
Maisha hayakuwa rahisi kwake. Wazazi wake walikuwa wakifanya kazi ndogo ndogo ili kumlipia ada na mahitaji ya shule. Lakini kijana huyo hakuwahi kukata tamaa. Alifaulu darasa baada ya darasa mpaka akafika chuo kikuu. Siku alipohitimu chuo kikuu familia yake ililia kwa furaha. Kijiji kizima kilijivunia kuona mtoto wao amefika mbali kiasi hicho.
Baada ya kuhitimu alipata nafasi ya kujitolea katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Alifanya kazi kwa moyo wote. Alikuwa mnyenyekevu, mwenye heshima na tayari kusaidia kila mtu. Watu wengi walimpenda kwa sababu ya bidii yake.
Kila siku alikuwa akisema “Siku moja nitapata kazi nzuri na nitawasaidia wazazi wangu wapumzike.” Siku moja kulikuwa na ziara ya Mkuu wa Mkoa kwenda kutembelea wananchi maeneo mbalimbali. Kijana huyo alijitolea kuandaa kazi za safari na kuongozana na msafara huo. Safari ilianza vizuri huku kila mtu akiwa na furaha. Lakini njiani kulitokea ajali mbaya sana.
Watu walikimbia kusaidia. Vilio vilisikika kila upande. Katika ajali hiyo kijana huyo alipoteza maisha. Habari zilipofika nyumbani familia yake ilipigwa na huzuni kubwa. Watu wa kijiji walilia sana wakisema.
“Alikuwa na ndoto kubwa sana alikuwa karibu kufanikiwa.”Siku za baadaye watu wengi waliendelea kumkumbuka. Walikumbuka bidii yake moyo wake wa kusaidia wengine na namna alivyopambana mpaka kufika chuo kikuu.
Ingawa maisha yake yaliishia ghafla juhudi zake zilibaki kuwa somo kwa vijana wengine. Wengi walianza kusoma kwa bidii wakisema.
“Kama aliweza kupambana mpaka kufika chuo kikuu basi nasi tunaweza.”
Ndoto yake ilionekana kuzima baada ya kifo chake lakini hamasa aliyowaachia wengine iliendelea kuishi mioyoni mwao milele.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment