Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Salma alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba aliyejitahidi sana shuleni. Alipenda kusoma na alijitahidi kufanya mazoezi ya kila somo lakini bado alikuwa na hofu kubwa kila mara mitihani inapokaribia. Aliogopa kukosea na mara nyingi alijikuta akiwaza
“Je, nikifeli itakuwaje?”
Mwaka wa masomo ulipofikia mwisho ilitangazwa kuwa siku ya kadi ya ripoti imewadia. Wanafunzi wote walifahamishwa kuwa wataitwa mmoja mmoja darasani kuchukua matokeo yao. Salma alihisi moyo wake ukidunda haraka. Alikaa nje ya darasa akitazama wenzake wakiingia na kutoka wakiwa na hisia tofauti wengine wakifurahi na wengine wakionekana wenye huzuni.
Rafiki yake Asha alikuja na kukaa pembeni yake. “Salma umejitahidi sana mwaka huu. Usiogope” Asha alimwambia kwa upole.Salma alitabasamu kidogo lakini bado alikuwa na wasiwasi mkubwa.
Hatimaye jina lake likaitwa. “Salma njoo uchukue kadi yako ya ripoti ” mwalimu alisema.
Salma aliingia darasani polepole mikono yake ikitetemeka kidogo. Alisimama mbele ya mwalimu akiwa kimya.Mwalimu alimpa kadi ya ripoti na kumtazama kwa tabasamu.
“Salma nimefurahishwa na juhudi zako mwaka huu.”
Salma alishika kadi kwa mikono miwili na kuifungua taratibu. Macho yake yakapita kwenye alama moja baada ya nyingine. Alishangaa kuona kuwa alama zake zilikuwa zimepanda sana kulinganisha na mitihani ya awali.
Kwa sekunde chache hakuamini alichokiona. Kisha tabasamu kubwa likatanda usoni mwake na machozi ya furaha yakaanza kumlengalenga.
Mwalimu alimwita pembeni na kumwambia “Umefanikiwa kwa sababu hukukata tamaa. Umebadilika kwa kujitahidi na kuomba msaada pale ulipohitaji.”
Salma alitoka darasani akiwa na furaha kubwa. Asha alimkimbilia na kumkumbatia. “Nimekuambia utakuwa sawa!” Asha alisema kwa furaha.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment