BAHATI YA MWISHO YA REHEMA

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Rehema alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliyekuwa hafanyi vizuri kwenye somo la Hisabati. Kila mtihani alipofanya alirudi nyumbani akiwa na huzuni kwa sababu alama zake zilikuwa chini.

Baada ya muda alianza kuamini kuwa hisabati siyo somo lake. Alimwambia rafiki yake

“Mimi siwezi kabisa hisabati nitaanguka tu kila mara.”

Rafiki yake alimjibu “Usikate tamaa labda unahitaji tu mazoezi zaidi.”

Siku moja mwalimu wa hisabati aliwaandikia wanafunzi kazi kubwa ya mazoezi ya nyumbani. Wanafunzi wengi waliifanya kwa urahisi lakini Rehema alikaa muda mrefu bila kuelewa.

Aliporudisha kazi yake kulikuwa na makosa mengi. Mwalimu alimwita pembeni na kumwambia

“Rehema si kwamba huwezi. Tatizo ni kwamba hujapata njia sahihi ya kujifunza.”Rehema alinyamaza lakini maneno yale yalibaki kichwani mwake muda mrefu.

Usiku ule aliamua kubadilika. Alianza kusoma polepole hatua kwa hatua. Kila aliposhindwa aliandika swali na kumuuliza mwalimu au rafiki zake siku inayofuata.

Siku nyingine alikaa na mwalimu baada ya masomo. “Mwalimu sielewi sehemu hii” alisema kwa ujasiri mdogo.Mwalimu alitabasamu na kumwelekeza kwa uvumilivu. Rehema alianza kuelewa kidogo kidogo. Wiki zilipita na Rehema akaanza kuona mabadiliko. Alama zake zikaanza kuongezeka taratibu. Ingawa bado hakikuwa rahisi sana hakujisikia tena kama hana uwezo.

Hatimaye mtihani mkuu wa muhula ulipofika Rehema alijitayarisha vizuri zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Alipomaliza mtihani alijisikia amefanya juhudi kubwa.

Baada ya matokeo kutoka alishangaa sana kuona amepata alama nzuri zaidi kuliko alizowahi kupata hapo awali.

Mwalimu alimwambia mbele ya darasa “Rehema ametuonesha kuwa mafanikio yanakuja kwa bidii na kutokata tamaa.” Rehema alitabasamu kwa furaha. Sasa alijua kuwa uwezo wake ulikuwepo alichohitaji ni uvumilivu na mazoezi.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments