Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Asubuhi ya mapema kabla hata jogoo hajawika mara ya pili mlango mdogo wa bati ulifunguliwa taratibu. Hapo ndipo tunapokutana na mtoto aitwaye Kadashi.
Kadashi aliishi na mama yake katika nyumba ndogo pembezoni mwa mji. Mama yake alikuwa mama lishe sokoni na kila siku aliamka mapema kwenda kuuza maandazi na chai. Kadashi alikuwa darasa la tano katika shule ya msingi ya karibu.
Maisha yao hayakuwa rahisi. Wakati mwingine walikosa umeme na Kadashi alisoma kwa mwanga wa kibatari au mshumaa. Lakini hakulalamika. Alijua mama yake alijitahidi sana ili apate ada, sare na daftari.
Siku moja shuleni mwalimu alitangaza kutakuwa na mtihani wa majaribio wiki iliyofuata. Wanafunzi wengi walionekana kujiamini lakini Kadashi alikuwa na wasiwasi. Hakukuwa na vitabu vya ziada nyumbani vya kumsaidia kufanya mazoezi.
Badala ya kukata tamaa Kadashi alianza kubaki darasani baada ya vipindi ili kumuuliza mwalimu maswali. Pia alisoma na rafiki yake Asha chini ya mti mkubwa karibu na shule. Walisaidiana kuelewa hesabu na kusoma kwa sauti masomo ya sayansi.
Siku ya mtihani ilipofika Kadashi alifanya kwa bidii kubwa. Wiki mbili baadaye matokeo yalipotangazwa Kadashi alikuwa wa pili darasani. Hakuruka kwa kelele lakini tabasamu lake lilionesha furaha ya kweli.
Aliporudi nyumbani na kumwonesha mama yake matokeo machozi ya furaha yalimtoka mama. “Ninajivunia sana juhudi zako” alisema kwa sauti ya upole.
Kadashi alijifunza kuwa mafanikio hayaji kwa miujiza bali kwa juhudi, nidhamu na kutokukata tamaa hata kama mazingira ni magumu.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment