Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Rehema alikuwa msichana mdogo aliyependa sana kusoma. Aliishi na wazazi wake katika familia maskini lakini ndoto yake ilikuwa kubwa alitaka kuwa mwalimu siku moja.
Kila siku Rehema alitembea umbali mrefu kwenda shule. Hata kama hakuwa na daftari la kutosha au kalamu nzuri hakukata tamaa. Alisikiliza kwa makini darasani na kufanya vizuri kuliko wanafunzi wengi.
Siku moja baba yake alipata ajali kazini na kuumia vibaya. Tangu siku hiyobhakuweza tena kufanya kazi. Hali ya familia ikawa ngumu sana. Mama yake alianza kufanya vibarua vidogo lakini pesa hazikutosha hata kwa chakula.
Baada ya muda wazazi wake walimwita Rehema na kumwambia kwa huzuni “Hatuwezi tena kumudu gharama za shule kwa sasa.”
Maneno yale yalimchoma moyo Rehema. Alihisi dunia yake imeanguka. Alilia usiku kucha akiwaza ndoto yake ya kuwa mwalimu ikitoweka polepole.
Siku iliyofuata hakwenda shule. Alibaki nyumbani akimsaidia mama yake kazi. Kila alipowaona watoto wengine wakipita na sare za shule machozi yalimtoka kimya kimya.
Lakini mwalimu wake aligundua kutokuwepo kwake. Baada ya siku chache alifika nyumbani kwao kujua kilichotokea. Aliposikia hali halisi aliguswa sana.
Kwa kushirikiana na watu wengine wa kijijini walichangisha fedha ili kumrudisha Rehema shule.
Siku aliporudi darasani alilia lakini safari hii machozi yalikuwa ya furaha.
Rehema alijifunza kuwa hata ndoto zinapovunjika bado zinaweza kujengwa tena kwa msaada wa wengine.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment