Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kulikuwa na mvulana mdogo aliyeitwa Kelvin aliyekuwa akiishi na baba yake katika mtaa wa kawaida mjini. Mama yake alikuwa amefariki miaka michache iliyopita na tangu siku hiyo maisha ya Kelvin yalibadilika sana.
Hapo zamani Kelvin alikuwa mtoto mwenye furaha sana. Alipenda kucheza mpira na marafiki zake, kucheka na kusimulia hadithi. Lakini baada ya kifo cha mama yake tabasamu lake lilianza kupotea polepole.
Baba yake alikuwa akifanya kazi muda mwingi ili kuhakikisha wanapata chakula na ada ya shule. Hii ilimfanya Kelvin abaki peke yake mara nyingi nyumbani. Hakukuwa na mtu wa kumsikiliza wala kumfariji kama zamani.
Siku moja shuleni mwalimu aliwauliza wanafunzi wachore picha ya kitu kinachowafanya wawe na furaha. Wanafunzi wengi walichora familia zao, marafiki au vitu wanavyopenda.
Kelvin alikaa kimya kwa muda mrefu. Mwishowe alichora picha ya mama yake akiwa amemshika mkono wote wakitabasamu.
Mwalimu alipokuja kuona kazi yake alinyamaza kwa muda. Aliona machozi yakianza kumtoka Kelvin taratibu. Kwa upole alimwuliza “Huyu ni nani?”
Kelvin alijibu kwa sauti ya chini “Ni mama yangu… alinifanya nitabasamu kila siku.”
Darasa lilitulia kimya wanafunzi wengine walimwangalia kwa huruma. Mwalimu alimkaribia na kumkumbatia kwa upole.
Kuanzia siku hiyo mwalimu alianza kumpa Kelvin muda zaidi na kumtia moyo. Pia aliwahamasisha wanafunzi wengine kuwa marafiki wa karibu na Kelvin.
Polepole Kelvin alianza kurudisha tabasamu lake ingawa hakuwahi kumsahau mama yake.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment