Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Ashurey alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mwanga. Aliishi na mama yake ambaye alikuwa mfanyabiashara mdogo sokoni. Maisha hayakuwa rahisi na mara nyingi Ashurey alienda shule bila chakula cha ziada kwa sababu mama yake hakuwa na uwezo wa kumwandalia kila siku.
Kila siku Ashurey alikaa pembeni akiwaangalia wenzake wakifungua mabakuli ya chakula wakati wa mapumzikou. Wengine walikuwa na maandazi, wali, ndizi au juisi. Harufu ya chakula ilimfanya Ashurey ahisi njaa zaidi.
Siku moja alimwona rafiki yake Juma akiwa na bakuli lililojaa maandazi. Juma alipokuwa anaongea na marafiki wengine Ashurey alisogea polepole. Moyo wake ulikuwa unadunda kwa kasi. Kwa haraka alichukua maandazi mawili na kuyaweka mfukoni mwa sketi yake.
Baada ya mapumziko Juma aligundua chakula chake kimepungua. Alimwambia mwalimu wa zamu. Mwalimu aliwaita wanafunzi wote na kuwauliza kwa utulivu.
“Kuna nani anayejua kilichotokea? ”Ashurey alikaa kimya lakini hakuweza kujisitiri. Alijisikia vibaya sana. Alikumbuka maneno ya mama yake aliyokuwa akisema mara nyingi.
“Mtoto wangu hata ukiwa na njaa usichukue cha mtu bila ruhusa.”
Machozi yakaanza kumtoka. Ashurey alisimama na kukiri kosa lake mbele ya darasa. Wanafunzi wengine walinyamaza. Mwalimu hakumkasirikia bali alimshukuru kwa kusema ukweli. Alimweleza Ashurey kuwa udokozi ni kosa lakini kusema ukweli ni hatua ya kwanza ya kujirekebisha.
Kuanzia siku hiyo mwalimu aliwahimiza wanafunzi kushirikiana chakula na shule ilianza kuwasaidia watoto waliokuwa na changamoto. Ashurey aliacha kabisa tabia ya kudokoa na akajifunza kuomba msaada pale anapohitaji.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment