Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika kijiji cha Bahari aliishi msichana mdogo aliyeitwa Tunu. Tunu alipenda sana kuogelea lakini aliogopa maji kwa sababu hakujua kuogelea vizuri.
Kila jioni alienda ufukweni kuwaangalia wavuvi wakivua samaki. Alitamani siku moja awe jasiri kama wao. Siku moja babu yake alimwambia
“Ujasiri hauji mara moja huanza kwa hatua ndogo.”
Kesho yake Tunu alianza kujifunza kuogelea kwenye maji mafupi akiwa na babu yake. Mwanzoni aliogopa lakini babu alimshika mkono na kumtia moyo. Kila siku alijifunza kidogo zaidi.
Siku moja wakati watoto wengine walipokuwa wakicheza karibu na maji mpira wao ulianguka baharini. Watoto wote waliogopa kuufuata. Tunu alikumbuka mafunzo ya babu yake. Akaingia kwa uangalifu kwenye maji na kuogelea taratibu hadi alipoufikia mpira. Akauleta ufukweni.
Watoto walimshangilia “Hongera Tunu! Wewe ni jasiri!”
Tunu alitabasamu aligundua kuwa ujasiri si kukosa hofu bali ni kufanya jambo jema hata kama unaogopa kidogo.
Tangu siku hiyo Tunu aliendelea kuwa jasiri na kusaidia wengine.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872

Post a Comment