REHEMA NA CHUPA YA MAJI

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Rehema alikuwa msichana wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Tumaini. Alikuwa mtoto mtiifu na mwenye tabia nzuri. Kila asubuhi mama yake alimkumbusha kubeba chupa yake ya maji kabla ya kwenda shuleni kwa sababu kunywa maji safi kulikuwa muhimu kwa afya.


Siku moja jua lilikuwa kali sana. Watoto walipokuwa wakicheza wakati wa mapumziko Rehema aliketi chini ya mti akinywa maji kidogo kidogo ili yasiishe haraka. Akiwa hapo alimwona mvulana mmoja mpya amekaa peke yake mbali na wenzake. Alikuwa anafuta jasho na kuonekana mchovu sana.

Rehema alimsogelea kwa upole na kumuuliza “Hujajiunga na wenzako kucheza una tatizo?”

Mvulana yule akajibu “Jina langu ni Baraka. Nimesahau chupa ya maji nyumbani na sasa nina kiu sana.”


Rehema alifikiria kwa muda. Alijua maji yake hayakuwa mengi lakini moyo wake haukumruhusu kumwacha Baraka aendelee kuteseka. Akamkabidhi chupa yake na kusema

“Kunywa kidogo nasi tuko pamoja.”

Baada ya hapo walikaa pamoja wakizungumza hadi kengele ya kuingia darasani ilipolia. Darasani Baraka alionekana mwenye furaha zaidi na aliweza kuzingatia masomo vizuri.

Siku iliyofuata Baraka alikuja shuleni na chupa mbili za maji. Moja alimpa Rehema akisema

“Asante kwa kunisaidia. Rafiki mwema hakusaha".

Rehema alitabasamu akajua kuwa wema mdogo unaweza kuleta urafiki mkubwa.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments