Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika jiji zuri lenye majengo marefu ya kisasa, barabara safi zenye taa zinazong’aa usiku na bustani nzuri za kupumzikia aliishi baba mmoja aitwaye Samson pamoja na watoto wake wawili July na Manuel
Walikuwa wanaishi katika nyumba nzuri ya ghorofa moja yenye maua na gari lililoegeshwa nje. Kila asubuhi jua lilipochomoza juu ya majengo ya jiji Samson aliamka mapema na kujiandaa kwenda kazini. Alifanya kazi katika ofisi kubwa katikati ya jiji. Alivaa suti nadhifu na kuaga watoto wake kwa tabasamu.
July na Manuel walikuwa wanasoma katika shule nzuri ya mjini. Kila siku walipanda gari la shule lililowachukua karibu na nyumbani kwao. Baada ya shule walirudi nyumbani na kufanya kazi zao za masomo kwenye chumba chao kizuri cha kusomea.
Jioni Samson aliporudi kutoka kazini familia ilikaa pamoja mezani kula chakula cha jioni. Walizungumza kuhusu siku yao walicheka na kushirikiana hadithi. Wakati mwingine walitoka pamoja kwenda bustanini au dukani kununua vitabu na vitu vya shule.
Siku moja Manuel alimuuliza baba yake
“Baba kwa nini unafanya kazi kwa bidii kila siku ilhali tuna kila kitu?”
Samson alitabasamu na kusema
“Maisha mazuri yanahitaji juhudi na uwajibikaji. Nafanya kazi kwa bidii ili muendelee kuishi vizuri msome vizuri na mtimize ndoto zenu.”
Watoto wake walimkumbatia kwa upendo. Walijua kuwa baba yao hakuwa anafanya kazi tu kwa ajili ya pesa bali kwa ajili ya furaha na ustawi wa familia yao.
Miaka ilipita July na Manuel walifaulu sana shuleni. Walimshukuru baba yao kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kuishi na kusoma.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment