Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika kijiji cha Mwembeni aliishi Mzee Hamisi pamoja na mke wake na mjukuu wake mdogo. Alikuwa na ng’ombe mmoja tu aliyeitwa Pendo ambaye alikuwa mali yao muhimu zaidi. Kila asubuhi Mzee Hamisi alikuwa anakamua maziwa na kuyauza ili kupata pesa ya chakula na ada ya shule ya mjukuu wake.
Siku moja Pendo akaanza kubadilika. Alikataa kula vizuri akawa mchovu na maziwa yakapungua sana. Mzee Hamisi akapata wasiwasi mkubwa. Bila maziwa maisha yangekuwa magumu zaidi.
Watoto wawili wa jirani Asha na Bakari walikuwa wakipita karibu kila siku. Walipoona Pendo hana nguvu walimwambia Mzee Hamisi
“Babu hebu tumsaidie. Huenda anahitaji kutunzwa zaidi.”
Kuanzia siku hiyo Asha na Bakari walianza kumsaidia. Walimpeleka Pendo malishoni penye majani mabichi walimhakikishia anapata maji safi na walimsafisha banda lake kila jioni. Walikuwa wakimzungumzia kwa upole kana kwamba anaelewa.
Baada ya wiki kadhaa Pendo akaanza kuonesha mabadiliko. Alianza kula vizuri akawa na nguvu na polepole maziwa yakarudi. Siku moja asubuhi Mzee Hamisi akashangaa kuona ndoo imejaa maziwa kama zamani.
Mzee Hamisi akafurahi sana. Aliwashukuru Asha na Bakari mbele ya watu wa kijiji akisema
“Upendo wenu kwa mnyama huyu umeokoa familia yangu.”
Tangu siku hiyo watoto wa kijiji walijifunza kuwajali wanyama na kuelewa kuwa wanyama nao huhitaji upendo na uangalizi.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment