Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Musa alikuwa mvulana wa miaka kumi aliyeishi na wazazi wake pamoja na dada yake mdogo Zawadi. Musa alipenda sana kucheza michezo kwenye simu na kuangalia runinga. Mara nyingi alisahau au alipuuza kazi za nyumbani alizopewa.
Kila jioni mama yake alimwambia “Musa tafadhali fanya kazi zako za nyumbani kabla ya kucheza.” Lakini Musa alikuwa akisema
“Nitafanya baadaye” na baadaye hiyo haikuwahi kufika.
Siku moja mama alipata uchovu mwingi na akaamua kupumzika. Vyombo vilijaa jikoni nyumba ikawa chafu na Zawadi alihitaji msaada wa kazi za shule. Baba alikuwa kazini hivyo jukumu lilimwangukia Musa.
Musa alikaa kimya akiitazama hali ya nyumbani. Aligundua kuwa bila yeye kusaidia mama angezidi kuchoka. Akasimama akaanza kuosha vyombo kufagia sebule na baadaye akamsaidia Zawadi kufanya kazi zake za shule.
Mama alipofika sebuleni na kuona nyumba ikiwa safi alishangaa sana.
“Asante Musa” alisema kwa furaha umenifanya nijisikie kupendwa.”
Musa alitabasamu. Alijisikia fahari kwa msaada alioutoa. Tangu siku hiyo Musa alianza kufanya kazi za nyumbani kwa hiari bila kukumbushwa. Nyumbani pakawa pa amani na furaha zaidi.
Funzo: Kuwajibika nyumbani huonyesha upendo na heshima kwa familia.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872

.jpeg)
Post a Comment