KUMWAMINI MUNGU HUONDOA HOFU

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Katika jiji la Daraja aliishi msichana mdogo aitwaye Shely. Aliishi na wazazi wake katika nyumba ya ghorofa karibu na barabara yenye magari mengi na taa zinazong’aa usiku.

Shely alikuwa mtoto mwenye furaha, lakini wakati mwingine aliogopa. Usiku alipokuwa akisikia sauti za magari na mbwa kubweka, moyo wake ulianza kudunda haraka. Shuleni pia, marafiki zake walipoongea kuhusu mambo ya kutisha, alihisi wasiwasi.

Siku moja baada ya kurudi kutoka shule alimwambia mama yake “Mama naogopa sana wakati mwingine.”

Mama yake akamkumbatia na kusema kwa upole“Mwanangu, kumbuka Mungu yuko pamoja nawe kila mahali nyumbani, shuleni hata njiani. Ukimwamini atakulinda.”

Maneno hayo yaliingia moyoni mwa Shely. Kuanzia siku hiyo alianza kuomba kila asubuhi kabla ya kwenda shule na kila usiku kabla ya kulala.

“Mungu wangu nakuamini. Nipe amani na ujasiri ” aliomba kwa sauti ya taratibu.

Polepole Shely akaanza kubadilika. Alipokuwa akisikia sauti za nje hakutetemeka tena. Alikumbuka kuwa Mungu ni mkubwa kuliko hofu yake.

Siku moja rafiki yake Neema alilia darasani kwa sababu aliogopa kulala peke yake. Shely akamkaribia na kumwambia

“Usiogope Mungu anakupenda sana jaribu kuomba kabla ya kulala.”

Neema akafanya hivyo na naye akapata amani moyoni.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872




0/Post a Comment/Comments