Mwanakwetukids
Akida alikuwa mvulana wa darasa la sita aliyependa sana kuchora. Kila alipokuwa na muda wa mapumziko alikaa chini ya mti wa kivuli shuleni na daftari lake mkononi. Alipenda kuchora nyumba, watu, wanyama na mandhari ya kijiji chao.
Lakini darasani Akida hakuwa wa kwanza katika masomo ya hesabu wala sayansi. Wakati matokeo yalipotoka mara nyingi jina lake halikuwa juu. Wanafunzi wengine walimcheka kimya kimya wakisema “Yeye anajua kuchora tu.” Maneno hayo yalimuumiza moyo lakini hakusema chochote.
Siku moja mwalimu wa sanaa alitangaza kuwa kutakuwa na mashindano ya kuchora kati ya shule zote katika wilaya. Kila darasa lilitakiwa kuchagua mwanafunzi mmoja. Wanafunzi wengi walitaka kushiriki lakini walipoulizwa nani anaweza kuchora vizuri baadhi yao walimtazama Akida.
Kwa mara ya kwanza Akida alihisi mchanganyiko wa hofu na furaha. Aliogopa kushindwa lakini pia alitamani kujaribu. Alipoenda nyumbani alimwambia mama yake kuhusu mashindano. Mama yake alimshika mkono na kumwambia
"Mwanangu jaribu kwa moyo wako wote. Ushindi si kila kitu muhimu ni kufanya bidii."
Siku ya mashindano ilipofika Akida alichora picha ya kijiji chao ambayo ni watoto wakicheza, wanawake wakichota maji kisimani na jua likichomoza nyuma ya milima. Alitumia muda wake wote kwa umakini mkubwa.
Wiki moja baadaye matokeo yalitangazwa. Akida hakushika nafasi ya kwanza lakini alipata tuzo ya “Mchoro wa Ubunifu Zaidi.” Shule nzima ilimpongeza. Wale waliomcheka awali walimwambia hongera.
Kuanzia siku hiyo Akida alianza kujiamini zaidi. Alielewa kuwa kila mtu ana kipaji chake na si lazima uwe bora katika kila somo ili uwe na thamani.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment