Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Neema alikuwa anaishi na bibi yake. Asubuhi nyingi alienda shule bila kifungua kinywa kwa sababu hali ya nyumbani ilikuwa ngumu.
Darasani wanafunzi wengi walikuwa wanakuja na vitafunwa maandazi, mikate au juisi. Wakati wa mapumziko kila mtu alikula.
Neema alikuwa anakaa pembeni akijifanya anacheza ili asionekane hana kitu.
Siku moja tumbo lilimuuma sana kwa njaa. Alikaa kimya huku akiwatazama wenzake wakila. Harufu ya mkate ilimfanya ashindwe kuvumilia.
Rafiki yake Asha alikuwa na mkate mkubwa. Alikula nusu tu kisha akaacha kipande mezani na kwenda kucheza.Neema alibaki karibu na dawati. Aliutazama ule mkate kwa muda mrefu…
Alichukua… akauweka tena… akauchukua tena…
Moyo ulimwambia: “Una njaa sana… hakuna atakayejua.” Lakini akakumbuka bibi yake alivyosema “Usichukue kisicho chako hata ukiwa na shida.” Neema akaondoka pale na kwenda kunywa maji mengi ili apunguze njaa.
Baadaye Asha aliporudi alikuta mkate wake bado upo. Alishangaa “Nilifikiri umechukuliwa.” Mwanafunzi aliyekuwa karibu akasema “Neema alikuwa hapa lakini hakugusa.” Asha akamfuata Neema nje. Akamkabidhi ule mkate “Najua ulikuwa na njaa… chukua. Huu ni wako nimekupa.”
Neema alishangaa “Lakini ni wako!”
Asha akatabasamu “Sasa ni wetu.”
Neema alikula huku macho yakijaa machozi si kwa njaa bali kwa furaha.
Jioni alimwambia bibi yake. Bibi akasema “Uaminifu huzaa baraka.” Kuanzia siku hiyo walikuwa wanashirikiana chakula kila siku.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment