Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Hapo zamani za kale kulikuwa na bahari kubwa sana iliyojaa samaki wa kila aina. Kulikuwa na samaki wakubwa wa kati na wadogo sana. Miongoni mwao aliishi samaki mdogo.
Alikuwa mdogo kuliko wote. Kila siku aliwaona samaki wakubwa wakicheza wakisafiri mbali na wakisaidia wengine. Yeye alikuwa akikaa pembeni akijiambia.
“Mimi ni mdogo sana siwezi kusaidia mtu yeyote.”
Siku moja asubuhi aliamka na kuona bahari imebadilika. Maji hayakuwa safi kama kawaida. Kulikuwa na plastiki, chupa na mifuko iliyokuwa ikielea kila mahali. Samaki wengi wakubwa waliogopa na kukimbilia mbali.
Akaogelea taratibu akitazama huku na kule. Ghafla akamsikia kaa akilia “Nisaidieni! Nimenasa!”
Akaona kaa amekwama ndani ya chupa ya plastiki. Alijua kazi ile ilikuwa ngumu lakini hakutaka kumuacha rafiki yake.
Akasema moyoni “Nitajaribu hata kama mimi ni mdogo.”Akaanza kuisukuma chupa ile polepole. Ilikuwa nzito lakini hakukata tamaa. Baada ya muda mrefu chupa ikageuka na kaa akaweza kutoka.Kaa akasema kwa furaha “Asante sana! Umenipa maisha mapya.”
Samaki wengine walipoona jambo lile walishangaa sana. Wakasema “Kama samaki mdogo anaweza kusaidia basi na sisi tunaweza!”
Samaki wakubwa na wadogo wakaungana. Walianza kusukuma takataka zote pembeni ya bahari. Ilikuwa kazi ngumu lakini walisaidiana kwa upendo na umoja.
Baada ya siku kadhaa bahari ikawa safi na nzuri tena. Mimea ya baharini ikaanza kukua na samaki wakaanza kucheza kwa furaha.
Samaki mdogo akatabasamu na kusema “Leo nimejifunza kuwa hata mdogo anaweza kufanya jambo kubwa.”
Tangu siku hiyo aliheshimiwa na samaki wote. Hakujidharau tena na bahari ikaendelea kuwa mahali pa furaha.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment