KUKU MREMBO NA YAI LA DHAHABU


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Kulikuwa na kijiji kizuri kilichoitwa Mawimbi. Katika kijiji hicho aliishi Bwana Juma mkulima mwenye moyo mwema lakini maskini sana. Siku moja alinunua kuku mmoja mrembo sokoni na kumpa jina Tunu. Alimpenda kuku wake na alimlisha vizuri kila siku.

Asubuhi moja Bwana Juma alipoingia banda la kuku aliona jambo la ajabu. Tunu alikuwa ametaga yai la dhahabu! Bwana Juma alilipiga msasa vizuri na kugundua kuwa lilikuwa la dhahabu halisi. Akaenda nalo sokoni na kulipata pesa nyingi.

Kuanzia siku hiyo kila siku Tunu alitaga yai moja la dhahabu. Bwana Juma alianza kujenga nyumba nzuri kununua nguo mpya na hata kuwasaidia majirani waliokuwa maskini. Kijiji kizima kilimpenda kwa wema wake.

Lakini baada ya muda tamaa ilianza kuingia moyoni mwa Bwana Juma. Alisema moyoni

“Kama Tunu anataga yai moja tu kwa siku ina maana ndani ya mwili wake kuna dhahabu nyingi zaidi. Nikimchinja leo nitapata utajiri wote mara moja!”

Siku iliyofuata kwa huzuni kidogo lakini akiwa na tamaa kubwa alimchinja kuku Tunu. Alipomfungua tumbo hakukuta hata chembe ya dhahabu. Alibaki na mikono mitupu.

Bwana Juma alianza kulia. Hakukuwa tena na mayai ya dhahabu. Alitambua kuwa tamaa yake imeharibu baraka aliyokuwa nayo.

Tangu siku hiyo aliwaambia watoto wa kijiji “Msiruhusu tamaa iwatawale. Baraka ndogo zikithaminiwa hukua kubwa.”

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments