AMINA NA MSITU WA SIRI

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Kulikuwa na kijiji kizuri kilichoitwa Kijiji cha Tumaini. Kijiji hicho kilizungukwa na msitu mkubwa sana uliokuwa na miti mirefu na ndege wa rangi mbalimbali. Wazee wa kijiji waliwaonya watoto wasikaribie sana msitu ule wakisema kuwa ulikuwa na siri nyingi za ajabu.

Katika kijiji hicho aliishi mtoto mmoja mchangamfu aliyeitwa Amina. Amina alipenda sana kusoma vitabu na kuuliza maswali mengi. Alitamani siku moja kugundua mambo mapya kuliko wengine.

Siku moja wakati akichunga mbuzi karibu na msitu aliona mwanga wa ajabu ukiwaka katikati ya miti. Alijaribu kupuuza lakini moyo wake ukamwambia “Nenda uone.”

Amina akaingia msituni polepole. Alipofika karibu na mwanga aliona mlango mdogo wa dhahabu kwenye shina la mti mkubwa. Juu ya mlango iliandikwa. "Wenye moyo mwema pekee ndio wanaoweza kuingia."

Amina akagonga mlango. Ghafla mlango ukafunguka na ndani akakuta kijana mdogo wa kichawi aliyevaa mavazi ya kijani.Kijana huyo akasema

“Karibu Amina. Mimi ni Mlinzi wa Msitu wa Siri. Msitu huu una hazina ya maarifa. Lakini ili uipewe lazima uthibitishe kuwa una moyo wa kusaidia wengine.”

Amina akauliza “Nifanye nini?”Mlinzi akamwonesha ndege mdogo aliyekuwa ameanguka na kuumia bawa.“Ukisaidia ndege huyu kwanza basi utastahili kuona hazina.”

Amina akamchukua ndege yule kwa upole akamfunga bawa kwa kitambaa chake na kumpa maji. Baada ya muda mfupi ndege akapata nguvu na akaruka tena angani.Mlinzi wa msitu akatabasamu.“Umefaulu. Sasa fuata njia hii.”

Amina akatembea hadi kwenye pango dogo. Ndani yake kulikuwa na vitabu vingi vya mwanga kila kimoja kiking’aa kama nyota. Mlinzi akasema “Hivi ni vitabu vya maarifa. Ukisoma na kuwafundisha wengine kijijini. Kijiji chenu kitakuwa bora.”

Amina akachukua kitabu kimoja na kurudi nyumbani. Kila siku alisoma na kuwafundisha watoto wengine. Baada ya muda watoto wote wakawa na akili na ujuzi mwingi. Kijiji cha Tumaini kikawa maarufu kwa elimu na maendeleo.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments