Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika kijiji kizuri kilichoitwa Mtoni aliishi mtoto mmoja aitwaye Abel. Abel alikuwa na miaka kumi na alikuwa maarufu kijijini kwa moyo wake wa huruma na ujasiri. Alipenda kusaidia wazee kucheza na wenzake na mara nyingi alisikia hadithi za wanyama wa porini kutoka kwa babu yake. Kila asubuhi Abel alikuwa akichunga mbuzi wa familia yake karibu na msitu uliokuwa pembeni ya kijiji. Alikuwa akipenda kuimba nyimbo wakati akichunga na mbuzi wake walimfuata kwa furaha.
Siku moja akiwa msituni alisikia sauti nzito ikisema “Guuuuu… Guuuu…!”
Abel alishtuka. Aliangalia pande zote akaona miti inatikisika. Aliposogea karibu alimwona ndovu mkubwa amekwama kwenye matope mazito. Ndovu alikuwa akijaribu kujinasua lakini alikuwa akizama zaidi.
Abel aliogopa kidogo lakini moyo wake wa huruma ulimshinda woga. Akasema
“Usihofu rafiki yangu. Nitatafuta msaada.” Alikimbia hadi kijijini na kuwaambia watu “Ndovu amekwama msituni! Lazima tumsaidie!” Baadhi ya watu waliogopa.
“Ndovu ni mkubwa sana anaweza kutudhuru” walisema. Lakini Abel akawajibu
“Kama hatutamsaidia ataumia zaidi. Tuwe wamoja.”
Hatimaye vijana na wazee wakakubali. Wakachukua kamba nene mapanga ya kukatia vichaka na ndoo za maji. Wote wakaelekea msituni pamoja na Abel.
Walipomfikia ndovu, walifunga kamba kwenye mwili wake kwa uangalifu. Wengine wakamwagilia maji kwenye matope ili yalainike. Kwa nguvu za pamoja wakavuta kwa nguvu kubwa.“Moja… mbili… tatu… VUTAAA!” wote walipiga kelele.
Baada ya kuvuta mara nyingi hatimaye ndovu akatoka kwenye matope! Ardhi ikatikisika kidogo na ndovu akasimama kwa nguvu. Ndovu aliinua mkonga wake juu na kupiga kelele ya furaha.
“Guuuuuu!” Kisha akamsogelea Abel akampapasa kichwa kwa mkonga wake kwa upole kana kwamba anasema asante. Watu wa kijiji walimshangilia Abel.
“Moyo wako wa huruma umetufundisha jambo kubwa” walisema.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
.jpg)
.jpg)
Post a Comment