NJIA NZURI YA KUMUADHIBU MTOTO ALIYEKOSEA

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Malezi bora ya mtoto yanahitaji nidhamu yenye upendo na hekima. Adhabu ni sehemu ya malezi lakini lazima itolewe kwa njia sahihi ili kumsaidia mtoto kujirekebisha si kumuumiza kimwili wala kisaikolojia. Njia nzuri ya kumuadhibu mtoto ni ile inayofundisha kurekebisha tabia na kujenga maadili mema.

Mzazi au mlezi anatakiwa kumweleza mtoto kosa lake kwa utulivu. Badala ya kupiga kelele au kumpiga ni muhimu kumwambia mtoto alikosea wapi na kwa nini kitendo chake hakikubaliki. Njia hii humsaidia mtoto kuelewa matokeo ya kosa lake na kujifunza kutofanya tena. Mtoto anapofahamu kosa lake huwa tayari kubadilika.

Adhabu isiyo ya kipigo ni njia bora zaidi. Mfano wa adhabu hizo ni kumnyima mtoto haki fulani kwa muda kama kucheza, kuangalia runinga au kutumia simu. Adhabu kama hizi humfundisha mtoto kuwajibika kwa matendo yake bila kuumizwa. Pia humsaidia mtoto kujifunza nidhamu na kujitawala.

Aidha kumsamehe mtoto baada ya adhabu ni jambo muhimu sana. Baada ya mtoto kuadhibiwa mzazi anapaswa kuonesha upendo na kumsihi asirudie kosa. Hii humfanya mtoto ajihisi kupendwa na kuthaminiwa hivyo kuwa tayari kurekebisha tabia yake.

Kwa kumalizia njia nzuri ya kumuadhibu mtoto ni ile inayojali haki, upendo na malezi bora. Adhabu haipaswi kuwa chanzo cha hofu bali iwe njia ya kumfundisha mtoto maadili mema na kumkuza kuwa raia mwema katika jamii.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments