Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika mtaa wa Tumaini mjini Iringa aliishi kijana mdogo aitwaye Juma mwenye umri wa miaka 10. Juma alikuwa mtoto mcheshi, mtiifu na mwenye bidii shuleni. Kila siku aliamka mapema ili kuwahi darasani ingawa walikuwa wanaishi kwenye nyumba ya kupanga yenye chumba kimoja tu.
Mama yake Juma alikuwa mama wa kuuza maandazi. Kila alfajiri kabla hata ya jua kuchomoza, alikuwa tayari jikoni akipika. Juma mara nyingi alimsaidia kupakia maandazi kwenye kikapu.
Siku moja mama yake alipoumwa ghafla asubuhi akaishiwa nguvu na kushindwa kuamka. Maandazi yalikuwa tayari lakini hakuna aliyeweza kuyapeleka sokoni.
Juma alibeba kikapu kikubwa akatembea haraka kuelekea sokoni. Barabarani kulikuwa na kelele za magari, pikipiki na watu wakikimbizana na shughuli zao
Alipofika sokoni baadhi ya wauzaji wakamcheka
“Mtoto kama wewe ataweza kweli kuuza maandazi?”
Lakini Juma hakukata tamaa. Alisimama sehemu tulivu na kupiga kelele
“Maandazi moto! Maandazi matamu ya mama Juma!”
Kwa mshangao wake watu walianza kusimama. Wengine walinunua kwa huruma wengine walipenda tu ladha ya maandazi yake.
Ilipofika saa nne asubuhi kikapu kilikuwa kimebaki kikiwa tupu. Juma aliuza kila kitu! Alikimbia kurudi nyumbani akiwa na tabasamu.
Kuanzia siku hiyo watu sokoni walimjua Juma. Mara kwa mara aliwasaidia wazazi wake na bado hakupoteza bidii ya masomo.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment