MCHEZO WA KURUKA JUU KWA WATOTO

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Mchezo wa kuruka juu ni miongoni mwa michezo muhimu sana kwa watoto hasa katika mazingira ya shule. Mchezo huu hufanyika kwa kuruka juu ya kamba, fito au utepe uliowekwa katika urefu fulani. Watoto hucheza mchezo huu kwa furaha kubwa huku wakijifunza mambo mbalimbali yanayosaidia katika ukuaji wao wa kimwili na kiakili.

Mchezo wa kuruka juu husaidia kuimarisha afya ya watoto. Kupitia kuruka misuli ya miguu na mikono huimarika na mwili mzima hupata mazoezi. Pia huongeza uwezo wa mtoto kufanya maamuzi ya haraka na kuwa na umakini.

Pia mchezo huu hujenga tabia njema kama ushirikiano, nidhamu na uvumilivu. Watoto hucheza kwa kupokezana zamu na kuheshimiana. Pia hujifunza kukubali kushinda au kushindwa bila ugomvi. Hali hii huwasaidia kujenga mahusiano mazuri na wenzao na kuwafanya wawe na roho ya michezo.

Vilevile mchezo wa kuruka juu huongeza kujiamini kwa watoto. Mtoto anapoweza kuruka juu zaidi kuliko awali hujisikia fahari na kupata moyo wa kujaribu mambo mapya. Hii huwasaidia hata katika masomo na shughuli nyingine za maisha.

Kwa ujumla mchezo wa kuruka juu ni muhimu sana kwa watoto. Unawasaidia kiafya, kijamii na kisaikolojia. Hivyo walimu na wazazi wanapaswa kuhimiza watoto kushiriki mchezo huu ili kuwajenga kuwa na afya njema, nidhamu na ujasiri katika maisha yao ya kila siku.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872




0/Post a Comment/Comments