URAFIKI WA SUNGURA NA KUKU

 


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Siku moja katika kijiji kidogo waliishi Kuku na Sungura waliokuwa marafiki wakubwa. Kila siku walicheza pamoja na kwenda kutafuta chakula msituni.

Siku moja mvua kubwa ilinyesha kwa muda mrefu. Mto uliokuwa karibu na kijiji ulifurika na kuharibu mashamba. Sungura alipoteza shimo lake alilokuwa akiishi na hakujua pa kwenda.

Akiwa amehuzunika Sungura alikimbilia kwa rafiki yake Kuku. Alipofika alisema kwa sauti ya huzuni,

“Rafiki yangu nyumba yangu imebomoka kwa maji. Sina pa kulala leo.”

Kuku alimwangalia na kusema kwa upole

“Usihofu rafiki yangu. Ingia kwangu tutalala pamoja. Nitakupatia nafaka zangu kidogo mpaka hali itakapotulia.”

Sungura alifurahi sana. Alikaa kwa Kuku kwa siku kadhaa hadi mvua ilipoisha. Baada ya muda Sungura alijenga shimo jipya. Lakini hakusahau wema wa rafiki yake.

Miezi michache baadaye Kuku alipougua na kushindwa kwenda kutafuta chakula Sungura alimtembelea kila siku na kumletea nafaka na maji. Alisema

“Rafiki mzuri hatasahau wema.”

Wote walifurahia urafiki wao hadi wakawa mfano kwa wanyama wote wa kijiji.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments