JE! FURAHA YA MTOTO INAJENGWA NA NINI?


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Furaha kwa watoto ni jambo muhimu sana katika maisha yao ya kila siku. Mtoto mwenye furaha hukua vizuri kimwili, kiakili na kihisia. Furaha huwajenga kuwa watu wanaojiamini wanaopenda kujifunza na wenye uwezo wa kuishi na wengine kwa upendo na ushirikiano.

 Furaha ya mtoto hutokana na upendo anaoupata nyumbani. Wazazi wanapompa mtoto upendo kumuelewa na kuzungumza naye kwa upole mtoto hujisikia salama na kuthaminiwa. Hii humsaidia kujenga tabia nzuri na kujiamini katika mazingira yote.

Pia michezo huchangia sana furaha ya mtoto. Kupitia michezo mtoto hujifunza kushirikiana kuunda mawazo mapya na kuimarisha afya yake. Michezo pia humsaidia mtoto kuachia msongo wa mawazo na kuwa na muda wa kufurahia utoto wake kikamilifu.

Aidha mtoto huwa na furaha anapopewa nafasi ya kusema mawazo yake na kusikilizwa. Kusikiliza mtoto humfanya ajue kwamba maoni yake ni muhimu. Hii humjenga kuwa na ujasiri na uwezo wa kuongea bila woga.

Lakini pia mazingira rafiki pia huongeza furaha ya mtoto. Mtoto anayekua katika mazingira salama yenye utaratibu mzuri na watu wanaomheshimu huishi kwa furaha na amani. Mazingira mabaya humfanya mtoto kuwa na hofu na kushindwa kuonesha uwezo wake.

Kwa ujumla furaha ya mtoto ni msingi wa maendeleo yake yote. Wazazi walezi na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa kwenye upendo, michezo, mawasiliano mazuri na mazingira salama. Mtoto mwenye furaha leo anakuwa mtu mzima bora kesho.


0/Post a Comment/Comments