Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Homa ya mapafu imeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya watoto wadogo, hasa wale walio chini ya umri wa miaka mitano. Ugonjwa huu wa kuambukiza unasababisha vifo vingi duniani, na hata nchini, wazazi wengi wamekuwa wakikumbwa na changamoto hii.
Mary Wanjiku Murimi mama wa watoto wanne anakumbuka kwa huzuni jinsi mwanawe wa pili alivyougua homa ya mapafu mara kadhaa. “Mtoto alianza kupumua kwa kasi kutoa sauti isiyo ya kawaida na kuwa dhaifu sana. Tulimkimbiza hospitalini ambako aliwekewa oksijeni na kugundulika kuwa na homa ya mapafu,” anasimulia Mary.
Mary anasema tukio hilo lilikuwa la kutisha kwani hakutarajia mwanawe kupata ugonjwa huo wakati ambao haukuwa msimu wa baridi. “Kumwona akiwa kwenye mashine ya oksijeni na akipumua kwa shida ilikuwa hali ya maumivu makubwa,” anasema kwa uchungu.
Kwa mujibu wa Dkt. Margaret Wainaina daktari bingwa wa watoto homa ya mapafu husababishwa na virusi, bakteria au kuvu (fungi) na mara nyingi huchochewa na ukosefu wa hewa safi. “Wazazi wanapaswa kuwa makini na dalili kama kupumua kwa haraka, homa ya juu na udhaifu wa ghafla. Matibabu ya mapema yanaweza kuokoa maisha ya mtoto,” anashauri.
Homa ya mapafu ni ugonjwa unaoweza kuzuilika lakini unahitaji uelewa tahadhari na hatua za haraka ili kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment