FAIDA ZA ASALI KWA WATOTO

 


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Asali ni chakula kitamu chenye virutubisho vingi vya asili. Imetumika kwa miaka mingi kama chakula na dawa. Kwa watoto asali ni muhimu sana kwani inasaidia katika ukuaji na afya njema ya mwili. Wazazi wengi hutumia asali kama tiba ya asili kwa watoto wao kwa sababu haina kemikali na ni salama kutumika baada ya mtoto kufikisha mwaka mmoja.

Kwanza asali husaidia kuimarisha kinga ya mwili. Watoto mara nyingi hupata maradhi kama mafua, homa na kikohozi. Asali ina virutubishi vinavyosaidia mwili wa mtoto kupambana na magonjwa haya. Kwa mfano mtoto anayekunywa maji ya uvuguvugu yenye asali ana uwezo mkubwa wa kukabiliana na maambukizi.

Pia asali hupunguza kikohozi na maumivu ya koo. Wazazi wengi hutumia asali kama dawa ya kikohozi kwa watoto wao. Kijiko kimoja cha asali kinaweza kupunguza muwasho kooni na kusaidia mtoto kulala vizuri usiku bila kukohoa sana. Ni tiba rahisi na ya asili ambayo haina madhara.

Asali huongeza nguvu mwilini. Asali ina sukari ya asili ambayo hutoa nishati kwa mwili. Watoto wanaotumia asali huwa na nguvu zaidi pia wanacheza na kujifunza vizuri shuleni. Kwa sababu hiyo asali ni bora kuliko pipi na vinywaji vyenye sukari nyingi.

Aidha asali huboresha usingizi wa mtoto. Mtoto akinywa maziwa yenye asali kabla ya kulala hupata usingizi mzuri na mwili wake hupumzika vizuri. Usingizi mzuri husaidia mtoto kukua kwa afya njema na kuwa na akili timamu.

Ni muhimu kujua kwamba asali haifai kutolewa kwa watoto walio chini ya mwaka mmoja. Hii ni kwa sababu miili yao bado ni dhaifu na inaweza kushindwa kupambana na bakteria fulani wanaopatikana kwenye asali mbichi. Kwa hiyo, watoto wa zaidi ya mwaka mmoja ndio wanaopaswa kupewa asali na kwa kiasi kidogo.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872.


0/Post a Comment/Comments