ASHA NA DAFTARI LA KALE

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Asha alikuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Mbuyuni. Alipenda kusoma lakini mara nyingi alikuwa akichelewa shuleni kwa sababu alihitaji kusaidia mama yake kuuza mboga sokoni kila asubuhi.

Siku moja Asha alipofika shuleni mwalimu wake Mwalimu Neema alimkemea kwa kuchelewa. Asha akahisi huzuni na akakaa kimya. Wakati wa mapumziko alikaa chini ya mti mkubwa wa kivuli nyuma ya madarasa. Akiwa amenyong’onyea akaona daftari la zamani limeanguka karibu na benchi.Akalipokea akafungua ukurasa wa kwanza na kukuta limeandikwa.

“Usikate tamaa. Kila siku ni nafasi mpya ya kufanya vizuri.”

Maneno hayo yalimgusa sana. Kila ukurasa wa daftari lilikuwa na maneno ya ushawishi kama vile “Kujituma ni siri ya mafanikio” na “Mafanikio madogo leo ni hatua kubwa kesho.”

Kuanzia siku hiyo Asha alianza kujitahidi zaidi. Aliamka mapema kusaidia mama yake kisha akaenda shuleni kwa wakati. Mwalimu Neema aliona mabadiliko hayo na akampongeza mbele ya darasa.

Miezi michache baadaye Asha alishika nafasi ya kwanza katika mtihani wa mwisho wa muhula! Wanafunzi wote wakashangilia. Mwalimu Neema akamwambia

“Asha nimejifunza kitu kutoka kwako kwamba mwanafunzi anayejituma hawezi kushindwa.”

Asha akatabasamu na kumwambia “Mwalimu nilijifunza kutoka kwa daftari la kale kwamba kila siku ni nafasi mpya ya kuanza upya.”

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments