UZURI WA MTU HAUONEKANI KWENYE MAVAZI

 Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Khalid alikuwa mtoto aliyependa kuvaa nguo nzuri na kujionyesha mbele ya wenzake. Kila asubuhi alipofika shuleni alisema kwa sauti "Angalieni viatu vyangu vipya! Hakuna anayenizidi hadhi hapa!"

Marafiki zake kama Asha na Baraka walimwambia "Mavazi siyo kila kitu cha muhimu ni moyo mwema." Lakini Khalid hakuwasikiliza. Alidhani kuwa nguo nzuri ndizo zinazomfanya kuwa bora kuliko wengine.

Siku moja shule yao ilipanga kwenda ziara ya kujifunza shambani. Watoto walivaa nguo rahisi kwa ajili ya kazi za shamba. Lakini Khalid alivaa suti yake mpya na viatu vya kung'aa. Alisema "Mimi siwezi kuvaa nguo hizi za kawaida kama ninyi."

Walipofika shambani walimu waliwaambia watoto wachimbe udongo na kupanda miche. Watoto wote walianza kufanya kazi kwa furaha isipokuwa Khalid. Viatu vyake vilianza kuteleza kwenye matope na nguo zake zikachafuka haraka.

Asha alimuambia "Njoo tukusaidie si vibaya kuchafuka unapojifunza." Lakini Khalid alikataa na kusema "Sitachafua nguo zangu kwa kazi hizi ndogo!"

Ghafla aliteleza na kuanguka kwenye matope! Watoto wote waligeuka na kumuona akiwa amejaa matope kuanzia kichwani hadi miguuni. Wote wakacheka kidogo sio kwa kumdharau bali kwa mshangao. Khalid alibaki kimya macho yakiwa na aibu.

Walimu walimnyanyua na kumsaidia kujisafisha. Mwalimu mkuu alisema kwa upole "Khalid nguo nzuri hazimaanishi kitu kama moyo hauna unyenyekevu. Leo umejifunza kuwa hakuna kazi ndogo na hakuna mtu anayeinuliwa na kiburi."

Kuanzia siku hiyo Khalid aliacha kujisifia. Alijifunza kufanya kazi pamoja na wenzake na akaelewa kuwa heshima ya kweli hutoka katika tabia njema sio mavazi.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments