USIWE RAHISI KUMUAMINI KILA MTU

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Kulikuwa na msichana mdogo aitwaye Linda. Linda aliishi na bibi yake katika kijiji kidogo kilichozungukwa na misitu na mito. Alikuwa mtoto mwenye tabasamu kila wakati na alipenda kusaidia watu.

Siku moja bibi yake alimwambia:

 “Linda tafadhali nenda sokoni uniletee unga wa mahindi na maziwa. Lakini kumbuka usisimame njiani kuzungumza na watu usiowajua.”

Linda akakubali kwa furaha akachukua kikapu chake na kuanza safari. Njiani alipokuwa akitembea alikutana na mbweha mjanja. Mbweha akamwuliza kwa upole.

 “Mtoto mzuri unaenda wapi peke yako?” Linda akakumbuka maneno ya bibi yake, lakini kwa kuwa mbweha alionekana mkarimu akajibu.

 “Naenda sokoni kumletea bibi yangu unga na maziwa.”

Mbweha akatabasamu na kusema

 “Acha nikuonyeshe njia ya mkato ili usichoke.”

Linda akakubali. Lakini kumbe mbweha alikuwa na hila! Alienda kwa haraka kupitia njia ya mkato halisi na kufika kwa bibi kabla ya Linda. Alijifanya kuwa Linda na akaingia ndani.

Bibi alipomuona akashangaa. “Linda kwa nini leo sauti yako ni tofauti?”

Kabla hajamaliza kuzungumza mbweha akakurupuka akitaka kumla bibi. Bahati nzuri Linda aliwasili wakati huo huo na kupiga kelele.

 “Watu wa kijiji! Msaada! Mbweha yuko kwa bibi yangu!”

Watu wa kijiji wakakimbia kwa haraka na kumfukuza mbweha mbali kabisa. Bibi akamkumbatia Linda na kumshukuru kwa ujasiri wake.

Tangu siku hiyo Linda alijifunza somo muhimu kutii wazazi na watu wazima na kuwa mwangalifu na watu usiowajua.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872



0/Post a Comment/Comments