UCHAPAKAZI HULETA MAFANIKIO


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Katika kijiji kizuri kilichozungukwa na milima na mashamba ya kijani aliishi msichana mdogo aitwaye Asha. Asha aliishi na mama yake ambaye alikuwa mkulima mwenye bidii. Kila siku asubuhi mama yake Asha alikuwa anaamka mapema kwenda shambani kulima mboga na mahindi.

Lakini Asha alikuwa tofauti. Yeye alipenda kulala hadi jua likiwa limechomoza sana na alipoamka alianza kucheza na marafiki zake badala ya kusaidia mama.

Siku moja mama yake akamwambia kwa upole.

“Asha mwanangu kama tunataka kula vizuri na kuwa na chakula cha kutosha lazima tufanye kazi kwa bidii.”

Lakini Asha akasema kwa kucheka.

 “Mama nitasaidia kesho leo nataka kucheza kwanza.”

Mama hakugombana naye. Alienda shambani peke yake na kuendelea kulima kwa bidii. Miezi ikapita mimea ikamea vizuri na matunda yakaanza kuiva.



Siku moja Asha aliporudi kutoka kucheza alihisi harufu nzuri ya matunda kutoka shambani. Akamkimbilia mama yake na kusema kwa furaha:

 “Mama matunda haya ni mazuri sana! Naomba nile kidogo.”

Mama akatabasamu na kumwambia kwa upendo:

“Binti yangu haya matunda ni zawadi ya kazi ya mikono yangu. Wewe hukusaidia kupanda kulima wala kumwagilia maji. Lakini kama unataka kula njoo leo unisaidie kuvuna.”

Asha akaona aibu alienda haraka kumsaidia mama yake kuvuna. Walipomaliza mama akamwambia.

“Unaona sasa? Matunda ni matamu zaidi ukiyapata kwa jasho lako mwenyewe.”

Tangu siku hiyo Asha alianza kuamka mapema kila siku na kumsaidia mama yake shambani. Walivuna mavuno mengi na maisha yao yakawa mazuri zaidi.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872

 

 

 

0/Post a Comment/Comments