TAI ALIYETAKA KUWA KAMA NDEGE WENGINE

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Kulikuwa na tai mdogo aliyeishi juu ya mlima mrefu. Tai huyu alikuwa mwenye nguvu, mwenye mabawa marefu lakini hakujua thamani yake.

Siku moja alishuka chini ya mlima na kukutana na ndege wengine wadogo kama ndege shamba, njiwa na kunguru. Akaanza kuwaangalia jinsi wanavyoruka kwa makundi huku wakiimba. Akaanza kufikiri:

 “Kwa nini mimi niruke juu peke yangu? Ningependa kuwa kama wao niruke chini na kucheza nao.”

Akaamua kuruka chini kabisa na kujaribu kuruka kama ndege hao wadogo. Lakini tatizo likatokea mabawa yake yalikuwa makubwa sana akajigonga kwenye miti akachoka haraka na akaruka hovyo.

Ndege wadogo wakamwambia kwa mshangao. “Wewe ni tai! Wewe umeumbwa kuruka juu zaidi ya mawingu. Ukijaribu kuwa kama sisi utateseka.”

Tai akasikitika. Akapanda tena juu ya mlima akaangalia anga kubwa na kusema

 “Labda kweli mimi nimeumbwa kwa ajili ya vitu vikubwa.”

Akapiga mabawa yake kwa nguvu… akaruka juu kuliko hapo awali akaona dunia yote chini yake kama ramani. Kwa mara ya kwanza alijisikia huru na mwenye furaha.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments