SUNGURA ALIYEJISIFU

 Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Kwenye msitu wa Furaha waliishi wanyama wengi waliopendana. Kulikuwa na Sungura aliyekuwa mwepesi kukimbia kuliko wote. Kila siku aliwaambia wanyama wengine,

“Hakuna mnyama anayenizidi kukimbia. Mimi ndiye bingwa wa msitu huu!”

Kobe ambaye alikuwa mtulivu na asiye na haraka alimwambia kwa sauti ya upole

“Sungura kasi si kila kitu. Unyenyekevu ni muhimu pia.”

Lakini Sungura alicheka na kusema. “WewMwepesi kama kobe? Hata nikiwa nimesinzia bado nitakushinda!”

Siku moja wanyama waliamua kufanya mashindano ya kukimbia kati ya Sungura na Kobe. Wanyama wote walikusanyika kuangalia. Twiga alikuwa mwamuzi akapiga filimbi na mashindano yakaanza!

Sungura alikimbia kwa kasi na kumwacha Kobe mbali sana. Akasema moyoni,

“Huyu kobe atanichukua miaka kumfikia. Wacha nipumzike kidogo.”

Akapumzika chini ya kivuli cha mti na akalala usingizi. Wakati huo Kobe aliendelea kutembea polepole bila kukata tamaa. Alipofika karibu na mwisho sungura akaamka na kukimbia kwa kasi lakini haikusaidia Kobe tayari alikuwa amevuka mstari wa mwisho.

Wanyama wote walimshangilia Kobe kwa uvumilivu wake. Sungura akainamisha kichwa kwa aibu.Kobe akasema kwa hekima.“Sio kasi tu inayomfanya mtu ashinde, bali nidhamu na unyenyekevu.”

Sungura akajibu kwa sauti ya unyenyekevu “Nimejifunza. Siwezi tena kujisifu Kuanzia leo nitaheshimu kila mmoja bila kujiona bora.”

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872



0/Post a Comment/Comments