Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kulikuwa na watoto wawili marafiki sana Juma na Tunda. Kila siku baada ya shule walipenda kwenda kando ya mto kucheza na kutazama ndege wakiruka. Karibu na mto kulikuwa na mti mkubwa wa matunda matamu lakini hakuna aliyewahi kuugusa kwa sababu watu walikuwa wakisema “Mti huu una siri.”
Watoto wengine walikuwa wakiogopa lakini siku moja Juma alisema
“Kwa nini tuogope? Labda mti huu unahitaji rafiki si mtu wa kuogopa.”
Wakakaribia mti kwa upole. Badala ya kuvuta matunda kwa nguvu kama wengine walivyojaribu zamani Tunda aligusa shina la mti na kusema kwa sauti ya upole
“Mti mzuri tunaomba matunda yako. Hatuji kuharibu tunataka tu kuonja kama marafiki.”
Ghafla upepo mwanana ukapita na matunda matatu yakadondoka chini taratibu kana kwamba mti umejibu. Juma na Tunda walishangaa na kufurahi sana. Walichukua matunda na kushukuru. Walipokula waligundua ni matamu kuliko matunda yote waliyowahi kuonja.
Tangu siku hiyo watoto wote walijifunza kuwa wapole na wenye heshima kwa mazingira na mti ule ukawa rafiki wa kijiji.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903972
Post a Comment