Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kulikuwa na simba mdogo aliyekuwa anaitwa Chekeni. Aliishi na familia yake katikati ya msitu mkubwa. Wakati wa mchana alikuwa mwenye furaha sana alikimbia alicheza na wanyama wengine na kupiga kelele kuonyesha ujasiri wake.
Lakini kila jua lilipozama hofu ilianza kumjaa. Giza likianza kuingia Chekeni aliogopa sana. Alijificha nyuma ya mwamba akitetemeka.
Siku moja mama yake alimwambia kwa upole.
“Chekeni usiogope giza. Giza si adui. Ndani ya giza kuna nyota zinazong’aa na mwezi unaotuliza moyo.”
Lakini Chekeni alitingisha kichwa “Lakini mama… ninaona vivuli vinaonekana kama viumbe vya ajabu!”
Mama yake alicheka kidogo akamkumbatia na kusema.
“Vivuli sio viumbe wabaya. Ni marafiki kimya wanaotuambia tuwe makini si tuogope.”
Usiku uliofuata Chekeni alijaribu kuwa jasiri. Alikaa karibu na mama yake na akajaribu kutazama angani. Akaona nyota zinavyometameta kama almasi. Akasikia upepo mwanana ukipita taratibu.
Ghafla akasikia “whooo… whooo…” akastuka!
Mama yake akasema “Huyo ni bundi anasema Usiogope Chekeni!'”
Taratibu alianza kutambua kuwa usiku ulikuwa mtulivu mzuri na wenye siri za kupendeza. Akapumua kwa utulivu na kulala usingizi mzuri kwa mara ya kwanza bila kujificha.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment