RAFIKI WA KWELI NI YULE ANAYE KUUNGA MKONO UNAPOHITAJI NGUVU

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Kulikuwa na wasichana wawili waliokuwa marafiki wa karibu sana. Walikuwa wanaitwa Hamida na Emma. Kila siku baada ya shule walipenda kukaa chini ya mti mkubwa karibu na uwanja wakizungumza kuhusu maisha na ndoto zao.

Hamida alitamani kuwa mwalimu ili awasaidie watoto kujifunza vizuri. Emma naye alitamani kuwa mwandishi wa habari maarufu atakayesimulia ukweli na kusimama kwa ajili ya haki.

Siku moja baadhi ya wanafunzi shuleni walianza kumcheka Emma kwa sababu daftari lake lilikuwa limechakaa. Wakamwambia kwa dharau.

 "Unawezaje kuwa mwandishi wa habari kama huna hata daftari zuri? Waandishi hutumia vitu vya kisasa!"

Emma alihuzunika sana. Hakuzungumza na mtu yeyote siku hiyo. Baada ya masomo hakwenda kucheza wala kuzungumza na Hamida kama kawaida. Aliondoka akiwa kimya.

Hamida aliyemjua vizuri rafiki yake alihisi kuwa kuna tatizo. Aliamua kumfuata hadi nyumbani. Alimkuta Emma amekaa kimya pembeni ya nyumba akiwa ameshika daftari lake lililochakaa.

Kwa sauti ya upole Hamida alisema "Emma uandishi wa habari si kuhusu daftari jipya. Ni kuhusu moyo wa kutaka kusema ukweli. Kama una ndoto usiache mtu yeyote hakukatishe tamaa."

Maneno hayo yalimgusa Emma. Alitabasamu kidogo na kusema.

 "Asante Hamida... wewe ni rafiki wa kweli."

Kesho yake shuleni Hamida alikaa karibu na Emma na wakacheka pamoja kama kawaida. Wanafunzi wengine walipoona jinsi walivyoshirikiana walijifunza kuwa ndoto hazitegemei vitu ulivyonavyo bali moyo ulionao na urafiki wa kweli ni kusaidiana na si kuchekana.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments