Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika mji mkubwa wa Daraja Kuu aliishi kijana mdogo aitwaye Pita pamoja na wazazi wake. Waliishi kwenye ghorofa nzuri karibu na shule yake. Kila siku asubuhi Pita alikuwa anakwenda shule akiwa amevalia sare safi, viatu vipya na begi lenye vitabu vizuri.
Kila alipokuwa akisubiri basi la shule alikuwa anamwona mtoto wa mtaa mmoja aitwaye Pato aliyekuwa anauza karanga barabarani ili kusaidia mama yake mgonjwa. Wanafunzi wengine walimcheka Pato kwa sababu nguo zake zilikuwa zimechakaa na miguu yake ilikuwa imejaa vumbi.
Lakini siku moja hali ikabadilika. Wakati Pita akisubiri basi mvua kubwa ilinyesha ghafla. Wanafunzi wengine walikimbia kujificha madukani lakini Pato alimkaribia Pita na kumfunika kwa kipande cha nailoni alichokuwa nacho.
“Asante sana Pato! Sikujua kama ungejali kunisaidia.”
Pato akatabasamu na kujibu kwa upole. “Sote ni binadamu ndugu yangu. Hata kama sina mengi bado naweza kusaidia.”
Maneno hayo yalimgusa Pita sana. Kuanzia siku hiyo alianza kumkaribia Pato zaidi. Kila asubuhi alimletea chakula kidogo au maji ya kunywa. Baadaye alimwambia mama yake kuhusu Pato na maisha yake magumu.
Mama yake Pita aliguswa na moyo wa huruma wa mwanawe. Akasema.
“Pita umefanya jambo la maana. Wacha tumsaidie Pato aende shule.”
Walizungumza na mkuu wa shule na Pato alipewa nafasi ya kusoma bure. Miezi michache baadaye Pato alianza kufanya vizuri sana darasani na yeye na Pita wakawa marafiki wa kweli wakisoma pamoja, kucheza pamoja na kusaidiana katika kila jambo.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment