Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kulikuwa na paka mmoja mdogo aitwaye Momo. Momo aliishi na bwana wake anayeitwa Juma kijana mwenye upendo mkubwa kwa wanyama. Kila siku Juma alimpa Momo maziwa na chakula kizuri.
Siku moja Juma alimwambia Momo “Usiingie jikoni bila ruhusa chakula cha watu si chako.”
Momo akaitikia kwa kichwa akiashiria kuelewa. Lakini ndani ya moyo wake alikuwa na tamaa.
Usiku ulipofika Juma akiwa amelala Momo alianza kunusa harufu ya samaki jikoni. Akashindwa kujizuia akaingia polepole. Akauma kipande kidogo na kukimbia. Juma alipoamka na kukuta chakula kimepungua alimuuliza Momo.
Momo alikataa kwa kugeuza uso akijifanya hajui jambo hilo.
Kesho yake jambo lile lile likatokea. Na tena Momo alikana. Taratibu Juma alianza kupoteza imani kwake. Hakumruhusu karibu na jikoni tena na hakumuamini alipokuwa kimya.
Siku moja paka mwingine kutoka nje aliingia ndani na kuiba chakula kingi jikoni. Momo alijaribu kumwambia Juma kwa sauti na ishara lakini Juma hakutaka kusikiliza akidhani Momo anafanya mchezo kama kawaida.
Baada ya wizi huo Momo alihuzunika sana. Akakaa mbele ya Juma macho yakiwa yamejaa majuto. Ndipo Juma akasema kwa upole. “Momo uaminifu ukipotea ni vigumu kurudisha. Ukisema ukweli tangu mwanzo ningekuamini leo.”
Tangu siku hiyo Momo alitoa sauti kila mara kwa uaminifu na hakuwahi tena kuiba au kusema uongo. Polepole Juma alianza kumwamini tena na urafiki wao ukarudi kama zamani.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment