Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika mji wenye pilikapilika nyingi magari yakipiga honi na watu wakikimbizana na majukumu aliishi msichana mdogo aitwaye Sarah. Alikuwa anasoma darasa la saba katika shule ya msingi iliyopo katikati ya mji.
Kila asubuhi Sarah alipokuwa akipita katikati ya majengo marefu na maduka alikuwa akiwaangalia watu wakifanya kazi mbalimbali.
Wengine wakiwa maofisini wakiwa na mavazi ya suti,Wengine wakiwa madereva wa magari ya huduma, Wengine wakipita na vitambulisho vya kazi shingoni na wanawake wakifungua mashine za saluni na vibanda vya urembo
Lakini kila alipoyaona hayo moyoni mwake swali moja liliendelea kurudi
“Mimi nikimaliza shule nitafanya kazi gani?”
Wakati mwingine Sarah alijiona akiwa daktari katika hospitali ya mjini akiwa amevaa koti jeupe.
Lakini mara nyingine akajiona akiwa mtangazaji kwenye televisheni akizungumza mbele ya kamera.
Siku nyingine alimtazama mama mwenye kioski cha vocha na juisi pembeni ya barabara na akawaza, “Labda naweza kuwa mfanyabiashara mkubwa na duka langu la kisasa.”
Siku moja alipokuwa akitoka shuleni alisimama kidogo karibu na mlinzi wa geti la shule mzee aliyekuwa mpole sana. Akamwambian “Mzee nikimaliza shule natamani kufanya kazi nzuri lakini sijui kama nitapata.”
Mlinzi akatabasamu akamwangalia Sarah kwa upole na kusema
“Mjini hapa watu wengi wanaamka asubuhi wakikimbizana na maisha lakini wachache wanafahamu wanataka kuwa nani. Kazi nzuri huanza pale unapojua kipaji chako. Shule inakupa macho lakini wewe mwenyewe ndiyo utaamua pa kutazama.”
Maneno hayo yalimgusa sana Sarah.
Kuanzia siku hiyo Sarah aliacha kuogopa swali la “nitafanya kazi gani” na akaanza kujiuliza swali jipya. “Ni kitu gani ninakipenda sana hadi naweza kukifanya bila kuchoka?”
Alianza kumwangalia kila mtu mjini kwa macho mapya si kama mtu tu anayefanya kazi bali kama mtu aliyechagua njia yake.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment