Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kulikuwa na sungura mdogo aliyekuwa akiitwa Fundi. Fundi alikuwa mjanja na mchangamfu lakini alikuwa na tabia moja mbaya hakupenda kusaidia wengine.
Siku moja wanyama wote wa msituni waliamua kujenga bwawa la maji ili wawe na sehemu ya kunywa wakati wa kiangazi. Twiga alileta miti mirefu, Tembo akachimba shimo kwa nguvu zake na Nyani akakusanya mawe. Kila mnyama alifanya kazi... isipokuwa Fundi Sungura ambaye alisema.
“Mimi ni mdogo siwezi kufanya kazi ngumu. Nitakuja tu kunywa maji mkimaliza!”
Wanyama waliumia moyoni lakini wakaendelea kufanya kazi bila malalamiko.Baada ya siku kadhaa bwawa likawa tayari na lilijaa maji safi. Wanyama walifurahi na wakaanza kunywa maji na kucheza pembeni ya bwawa. Fundi naye akaja mbio akisema.
“Ngoja ninywe maji yangu bwawa ni letu sote!”
Lakini alipofika aliambiwa na Tembo kwa upole. “Fundi maji haya ni ya wale waliotoa jasho. Hata maji kidogo unastahili lakini kwanza fanya kazi ndogo ya kusaidia.”
Walimpa kazi ya kukusanya vijiti ili kuimarisha ukingo wa bwawa. Fundi akaanza kukusanya akiwa amekunja uso lakini kadiri alivyofanya kazi alihisi furaha ya kushirikiana na wengine. Baada ya kumaliza aliruhusiwa kunywa maji na wanyama wote wakashangilia pamoja.
Tangu siku hiyo Fundi alijifunza thamani ya ushirikiano na hakuwahi kukataa kusaidia tena.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment