Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika dunia ya sasa iliyojaa maendeleo ya teknolojia simu imekuwa kifaa muhimu kinachotumiwa na watu karibu wa rika zote. Hata hivyo jambo linalozua mjadala ni kama ni sahihi mtoto kutumia simu. Wapo wanaoona simu inaleta manufaa na wapo wanaoamini inaleta madhara. Ili kupata jibu sahihi ni muhimu kuchunguza matumizi ya simu kwa mtoto kwa upande wa faida na hasara.
Kwa upande wa manufaa simu inaweza kuwa chombo cha elimu kwa mtoto. Kupitia programu za kujifunza mtoto anaweza kufahamu herufi, namba na hata lugha nyingine kwa njia rahisi na ya kuvutia. Vilevile simu humsaidia mzazi kuwasiliana na mtoto wake akiwa shuleni au safarini jambo linaloongeza usalama. Kwa njia hii simu inaweza kuwa msaada mkubwa ikiwa inatumika kwa malengo mazuri na yenye tija.
Kwa upande mwingine simu inaweza kuwa na athari mbaya kwa mtoto kama haitadhibitiwa. Baadhi ya watoto hutumia simu kuangalia video zisizofaa maadili kucheza michezo kupita kiasi na kusahau kusoma au kushiriki michezo ya nje. Hali hii inaweza kusababisha mtoto kuwa mvivu, kupoteza maadili na hata kuathiri afya ya macho pamoja na akili. Hivyo matumizi mabaya ya simu yanaweza kuharibu tabia na maendeleo ya mtoto.
Simu siyo mbaya illa matumizi yake bila usimamizi ndiyo huleta madhara. Ikiwa mzazi ataweka mipaka na kuhakikisha simu inatumika kwa elimu na mawasiliano muhimu tu basi matumizi ya simu kwa mtoto yanaweza kuwa sahihi. Lakini bila udhibiti simu inaweza kuwa chanzo cha kuporomoka kwa maadili na uwezo wa kujifunza.
Je, wazazi wa leo wanadhibiti matumizi ya simu kwa watoto au wamewaachia huru kupita kiasi?
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment