Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kulikuwa na kijana mmoja wa mjini aitwaye Bambo, aliyependa sana kula ndizi kuliko chakula kingine chochote. Kila siku alipita sokoni na kusema:
“Mimi ni bingwa wa ndizi duniani! Hakuna ndizi ninayoshindwa kuimaliza!”
Siku moja mama mmoja wa sokoni aliyekuwa mchokozi akamwambia
“Kama kweli wewe ni bingwa basi kula hizi ndizi tatu bila kucheka.”
Bambo akajifanya mwanaume jasiri akakaa kwenye benchi akachukua ndizi ya kwanza. Kabla hajaanza kula yule mama akapiga filimbi na watoto wote wakamzunguka wakisema.
“BINGWA WA NDIZI! BINGWA WA NDIZI!”
Bambo akajiziba masikio na kuanza kula. Alipofika kwenye ndizi ya pili mtoto mmoja akamuuliza kwa sauti kali:
“Kaka ukimaliza tutakupa tuzo ya ndizi za kesho pia?”
Bambo akacheka kidogo lakini akajikaza. Alipoanza ndizi ya tatu ghafla sokoni pakapita punda akiwa amefungwa ndoo ya ndizi shingoni. Yule punda akamwangalia Bambo na pua zikitoa sauti kama “Huuuuuu!” kana kwamba anamuambia "Bingwa wa kweli ni mimi!”
Watoto wakaanza kupiga kelele. “Bambo punda anakudharau!”
Hapo Bambo akashindwa kujizuia akacheka mpaka ndizi ikadondoka chini!
Mama wa sokoni akapiga makofi na kusema
“Bingwa wa ndizi… wa kuangusha ndizi!” Na kuanzia siku hiyo watu wote sokoni walimwita
“Bambo Bingwa wa kuangusha ndizi".
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment