UZURI SI RANGI BALI NI TABIA NJEMA


Emakulata Msafiri

Aliishi kanga mmoja aitwaye Kiki. Kiki alikuwa na manyoya mazuri yenye madoa ya rangi tofauti tofauti madoa ya buluu, ya kijani, ya manjano na mekundu. Wanyama wote walimshangaa kwa uzuri wake.

Lakini Kiki hakuwa na tabia nzuri. Alijivuna sana kwa sababu ya madoa yake. Alikuwa akiwaambia wanyama wengine.

"Mimi ni mrembo kuliko nyote! Angalieni manyoya yangu ya rangi! Hamfiki hata robo yangu!"

Twiga, sungura na tumbili walihuzunika lakini hawakusema chochote. Walijaribu kumkaribisha Kiki kucheza nao lakini Kiki alisema,

"Sichezi na wanyama wasio na rangi nzuri kama mimi!"

Siku moja mvua kubwa ilinyesha sana hadi kukawepo na mafuriko. Wanyama wadogo walikwama kwenye mti maji yakiwa yanapanda haraka. Kiki alikuwa juu ya mti mkubwa salama kabisa lakini hakuwa tayari kuwasaidia wenzake.

Twiga japo hakuwa na rangi nyingi alitumia shingo yake ndefu kuwavuta wanyama juu ya mti. Tumbili alirukaruka akiwasaidia watoto wa sungura kupanda juu. Hata kobe alimsaidia ndege mdogo aliyetokwa na nguvu.

Baada ya mvua kuisha wanyama walimshukuru Twiga, Tumbili na Kobe kwa moyo wa upendo na usaidizi wao. Kiki alibaki kimya.

Aliangalia madoa yake ya rangi na akasema kwa huzuni,

"Uzuri wangu haukuwa na maana kama siwezi kusaidia wengine."



Tangu siku hiyo Kiki alibadilika. Alicheza na wenzake, aliwasaidia na akawa rafiki wa wote si kwa sababu ya madoa yake bali kwa sababu ya moyo wake mpya wa upendo na unyenyekevu.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments